Thursday, 28 September 2017

TAARIFA KWA UMMA: OPERESHENI KA-MA-TA MWENDOKASI USIKU




Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Jeshi la Polisi(SACP) Fortunatus M. Musilimu,  akizungumza na waandishi wa habari juu ya Operesheni Ka-Ma-Ta aliyoianzisha hivi karibuni inayokusudia zaidi ukamataji wa Mabasi ya Abiria nyakati za usiku.




JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
                          JESHI LA POLISI TANZANIA
 


  TAARIFA KWA UMMA

       1.0 UTANGULIZI
Katika kukabiliana na Ajali za Barabarani, ambazo zimekuwa zikitokea na kusababisha Vifo na Majeruhi, kutokana na uzembe wa Madereva wasizingatia Sheria, Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, linafanya Operesheni kali ya kuwakamata madereva wasiozingatia sheria na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kufungia leseni zao.

Operesheni hii, sasa inafanyika Usiku na Mchana baada ya kubaini kuwa Madereva wa Mabasi ya Abiria wanaendesha kwa mwendo kasi kufidia muda wa mchana ambao hawakimbii kutokana na kudhibitiwa na Tochi za mwendo kasi kwa kuamini kuwa Usiku Tochi hazikamati na Askari wa Usalama Barabarani hawapo Barabarani na hivyo hawawezi kukamatwa.
Operesheni hii inafanyika sanjari na utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa hivi karibuni kuwataka madereva kutoendesha magari kwa mwendo kasi, wakati wa ufunguzi wa barabara mpya huko Simanjiro.
Jeshi la Polisi linatoa shukrani kwa wananchi kwa ushirikiano na kwa taarifa ambazo wamekuwa wakitoa na kuweza kusaidia kuwakamata madereva wanaofanya makosa barabarani.

      2.0   MAKOSA YALIYOKAMATWA
Katika Operesheni inayofanyika, kwa kipindi cha Wiki Moja, kuanzia tarehe 18 – 24/09/2017 tangu kuanza Operesheni hii jumla ya makosa 53,870 ya magari yamekamatwa. Idadi hii ya makossa yaliyokamatwa na idadi ya makosa 53,053 yaliyokamatwa katika kipindi hiki cha wiki moja kuanzia tarehe 11 – 17/09/2017 kabla ya Operesheni haijaanza, inaonyesha kuwepo kwa ongezeko la jumla ya makosa 817 yaliyokamatwa. Hivyo ukamataji wa makosa umeongezeka.

  
      3.0   OPERESHENI INAYOFANYIKA USIKU

Katika Operesheni inayofanyika Usiku jumla ya Madereva Saba (7) wa Mabasi yamekamatwa kwa kuendesha kwa mwendo kasi na hatarishi wa zaidi ya kilomita 90 kwa saa (90 km/hrs). Madereva walikamatwa waliwekwa mahabusu na kupelekwa mahakamani ambapo walikiri kosa na kutiwa hatiani kulipa faini kati ya Tshs. 100,000/- hadi 300,000/-. Kwa kutiwa hatiani madereva hao wamepoteza sifa ya kuendesha magari ya abiria kibiashara.

Kwa Mamlaka niliyopewa kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Tangazo la Serikali Na.31 la mwaka 2015, Kanuni Na.5 ya Sheria hiyo, nafuta madaraja “C” na “E” katika leseni za Madereva hao na hivyo hawataruhusiwa tena kuendesha magari ya abiria na mizigo kibiashara kwa kipindi cha Miezi Sita (6) mpaka warudi darasani wakasome, watahiniwe tena mpaka wafaulu ndipo warejeshewe madaraja hayo.






Madereva hao ni:-
1. HAMAD SHABANI SALUM, mwenye leseni Na.4001852854
2. KIJA ALOYCE MAYENGA, mwenye leseni Na. 4001518000
3. ISACK JOHN MBIJINA, mwenye leseni Na. 4000220395
4. HASSAN ABASI SEMAZUA, mwenye leseni Na. 4001522366
5. STANLEY JOSEPH MOSHA, mwenye leseni Na. 4000369436
6. ABDALLAH HUSSEIN, mwenye Leseni Na. 4000482412 – huyu yuko Mahabusu.
7. SEMPUNDA YUSUFU, mwenye leseni Na. 1-1980- 80006515226,
Aidha, dereva ISMAIL MOHAMED NYAMI, mwenye leseni Na. 4000676285, aliyesababisha ajali tarehe 23/09/2017 iliyoua watu 2 na kujeruhi watu 42 Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Dereva MSEKA HERMAN SALUM, mwenye leseni 4000118648 aliyesababisha ajali tarehe 25/09/2017 iliyoua mtu 1 na kujeruhi wengine 25 katika eneo la Maganzo, Wilaya ya Kishapu, Mkoani Shinyanga na Dereva MALICK HAMIDU HASSAN, mwenye leseni Na. 4000450337, aliyesababisha ajali ya kugonga Ng’ombe usiku na kupinduka, tarehe 21/09/2017 na kusababisha Kifo cha mtu 1 na majeruhi 6, hao nao leseni zao zimefungiwa na hawataruhusiwa kuendesha magari ya kubeba abiria.

Madereva wote hao waliofungiwa leseni, Waajiri wao watajulishwa na hivyo hawaruhusiwi kuendesha tena Mabasi. Pia Chama cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA), Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) nao watajulishwa kufungiwa kwa leseni hizo kwa hatua zaidi.


4.0 MABASI YALIYOFUNGIWA
Kwa kusirikiana na SUMATRA, kwa mujibu wa  kifungu cha 15 cha Sheria ya SUMATRA, jumla ya mabasi 11 ya Makampuni mbalimbali yamefungiwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwa makosa ya mwendokasi mpaka wahakikishe vifaa vilivyofungwa katika Magari yao vya kudhibiti Mwendo kasi vinafanya kazi. Makampuni hayo ya Mabasi tayari yamejulishwa kufungiwa kutoa huduma.


 
5.0 MAFANIKIO YA OPERESHENI
Operesheni inaonyesha mwelekeo wa kupungua kwa matukio ya Ajali, Vifo na Majeruhi. Kwa mfano kuanzia tarehe 18-24/9/2017 tangu Operesheni hii ianze, kumetokea jumla ya Ajali 37, Vifo 26 na Majeruhi 54. Ukulinganisha takwimu hizo na kipindi kama hicho kuanzia tarehe 11-17/9/2017 kabla ya operesheni hii kuanza, ambapo zilitokea jumla ya Ajali 66, Vifo 42 na Majeruhi 107 zinaonyesha kuwepo kwa Upungufu wa Ajali 29 ambazo ni sawa na 44%, Upungufu wa Vifo 16 ambavyo ni sawa na asilimia 38% na Upungufu wa Majeruhi 53 ambao ni sawa na asilimia 50%.

Aidha, Wananchi wengi wanaunga mkono hatua zinazochukuliwa dhidi ya madereva wasiozingatia sheria na kutaka operesheni hii iwe ya kudumu na endelevu.

Pia hofu ya watu kusafiri kwa mabasi kutokuwa na uhakika wa kufika salama imepungua. Wengi waliokuwa wameacha kupanda Mabasi kwa kuhofia kupata Ajali sasa wameanza kupanda Mabasi


6.0 RAI
 MADEREVA.
Madereva wazingatie sheria, wajenge utii wa sheria bila shuruti, wasisubiri kushurutishwa, waache kuendesha kwa mazoea na wabadilike. Wajue kuwa watakaofanya makosa barabarani watakamatwa palepale na kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufungiwa leseni.

Aidha, ieleweke kwamba, kwa makosa hatarishi, hatutatoza faini kwa njia ya Tozo la Notification. Tutawakamata madereva, kuwaweka mahabusu, kuwapeleka mahakamani na kufungia leseni zao. Madereva wajue kwamba kama udereva umewashinda, waache watafute kazi nyingine. Hatuwezi kukubali kuona Watanzania wanaendelea kufa na kujeruhiwa kutokana na ajali zinazosababishwa na madereva wazembe.
Pia Madereva watambue kwamba operesheni hii ni ya kudumu na endelevu na itafanyika muda wote, Usiku na Mchana. Wasidanganyike kuwa tochi zetu hazikamati usiku. Na kwamba Askari hawapo Barabarani. Tutawakamata muda wote na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria na kufungia Leseni zao mara moja.


ABIRIA
Abiria watoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapoona dereva anakiuka sheria. Abiria wasikubali kufaulishwa na kupakiwa katika mabasi yaliyojaa.

Aidha, Wasisubiri ajali itokee ndipo waanze kusema dereva alikuwa anaendesha kwa mwendo kasi na kwamba walikuwa wamezidishwa katika mabasi.

  ASKARI WA USALAMA BARABARANI
Watafanya kazi kwa kuzingatia Sheria, haki, maadili, huduma bora kwa mteja na hawatabambikizia mtu makosa.

7.0 HITIMISHO
Dereva yeyote aliyepewa leseni ya udereva bila kujali anaendesha gari ya aina gani, azingatie sheria vinginevyo atakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria na leseni yake itafungiwa. Kwa Operesheni hii na kasi hii dereva asiyetii Sheria hatabaki Salama.


“HATUTAKI AJALI, TUNATAKA KUISHI SALAMA”
Imetolewa na:-

(FORTUNATUS MUSILIMU)
KAMISHNA MSAIDIZI MWANDAMIZI WA POLISI (SACP)
 KAMANDA WA KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI (T)
TAREHE 28/09/2017